Thursday, September 25, 2025

HALI YA HEWA YA MKOA WA SINGIDA YATAKIWA KUTUMIWA KAMA FURSA NA SIO KIKWAZO



Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. FatumaMganga, amewataka viongozi na wadau wote wakilimo mkoani hapa kuweka mikakati thabiti yakuwaelimisha wakulima ili waweze kuingia na kuchochea mpango wa kilimo hai kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao maradufu.

Dk. Mganga amesema hayo wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, katika ufunguzi wa mkutano wa wadau wa kilimo (Multi-Stakeholder Dialogue) uliofanyika mjini Singida.

Mkutano huo ulihusisha viongozi wa serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), na wakulima, ambapo wadau walijadiliana juu ya fursa na changamoto za kilimo endelevu, kwa kuzingatia nguzo tatu kuu: watu (people), mazingira (nature), na uchumi (economy).

Akizungumza kwenye kikao hicho, Dkt. Mganga amesema Mkoa wa Singida ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa mazao ya biashara na chakula nchini, ikiwemo alizeti, pamba, karanga na mahindi, hivyo iwapo mikakati thabiti itawekwa ya kuwaingiza wakulima katika mpango wa kilimo hai, kutaongeza uzalishaji na kulinda mazingira ya mkoa huo.

Kwa upande wao, wakulima walioshiriki mkutano huo walieleza furaha yao kushirikishwa moja kwa moja katika majadiliano, jambo walilosema linaongeza uelewa na nafasi yao kushiriki katika mchakato wa kutengeneza sera za kilimo ngazi ya mkoa.


“Leo nimefurahishwa sana kuona sisi wakulima wa Singida tumewekwa pamoja na serikali, sekta binafsi na mashirika kama HELVETAS Tanzania. Kupitia mazungumzo haya tumejifunza njia za kulima kijani zinazolinda ardhi na maji, huku pia zikiongeza kipato chetu. HELVETAS na wadau wengine wametufundisha mbinu bora, wametupa mbegu na hata kutuunganisha na masoko. Mimi binafsi nimeona mavuno yangu yakiongezeka na ninaamini Singida inaweza kuwa kiongozi wa kilimo hai Tanzania.”

Mashirika yaliyojitokeza kushirikiana na serikali na wakulima katika kikao hicho ni pamoja na Regenerative Production Landscape Collaborative (RPLC), Laudes Foundation, GIZ na HELVETAS Tanzania, ambapo wote walionesha dhamira ya kusaidia wakulima kupitia elimu, teknolojia, na sera shirikishi zinazochochea kilimo cha kijani.



 



Wednesday, September 24, 2025

MRADI WA UMWAGILIAJI IRAMBA,WAKULIMA SHIDA YA MAJI KUISHA

Mradi wa Umwagiliaji wa Masimba unaotekelezwa katika vijiji vya Urughu na Masimba, kata ya Ndago, wilayani Iramba mkoani Singida, unaendelea na  utekelezaji wake huku ukitarajiwa kuwanufaisha wakulima wengi zaidi.

Mradi huu unajumuisha kazi za barabara za mashambani zimekamilika kwa asilimia 90.58, ambapo usafishaji na uwekaji wa vifusi jumla ya kilomita 21.67 umekamilika, huku kilomita 5.6 kati ya 9.25 za barabara zikiwa tayari. Kazi za maumbo ya umwagiliaji zipo kwenye asilimia 18.32, zikiwemo ujenzi wa vipunguza kasi 14 kati ya 47 na kalvati moja kati ya 25, wakati maandalizi ya mashamba yamefikia asilimia 16.93, ambapo hekta 132 kati ya 750 zimeshasawazishwa huku Mradi huu unagharimu shilingi bilioni 10.4 

Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Meneja wa Mradi Mhandisi Emmanuel Challo, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiamini Tume na kuipatia fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji ikiwemo huu wa Masimba.

Mradi huo wenye jumla ya ekari 1800 unatarajiwa kunufaisha wakulima 730 kupitia ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji.


Timu ya ukaguzi wa mkoa ikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, imependekeza kuongeza idadi ya watendaji wa mradi ili kazi zifanyike kwa kasi zaidi usiku na mchana, na hivyo wananchi waanze kunufaika mapema na mradi huo muhimu.























SONGAMBELE WAGUSWA UJENZI MADARASA NA NYUMBA ZA WAALIMU.

 

Ujenzi wa Nyumba ya Mwalimu 2 in 1 katika Shule ya Msingi Ushora ukiendelea.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, leo amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya elimu katika Wilaya ya Iramba, akiwa ameambatana na timu ya ufuatiliaji ya Mkoa.

Akiwa katika Shule ya Msingi Ushora Utemini, kijiji cha Songambele, Kata ya Ndago, Katibu Tawala alikagua mradi wa ujenzi wa madarasa matatu, matundu sita ya vyoo pamoja na vyumba viwili vya  madarasa ya awali  na matundu aita ya vyoo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 143 kupitia fedha za BOOST. Mradi huo upo katika hatua za awali za maandalizi ambapo mchanga, kokoto na tofali tayari vimekusanywa, huku michango ya wananchi ikiendelea.

Aidha, Katibu Tawala alitembelea mradi mwingine wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa 2-in-1 katika shule hiyo, mradi wenye thamani ya shilingi milioni 95 zilizotolewa na Serikali Kuu na nguvu kazi ya wananchi. Hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 53 zimetumika na kiasi cha shilingi milioni 44 kimebaki.

Mapendekezo yaliyotolewa baada ya ukaguzi huo uliofanyika ni pamoja na kuwataka viongozi wa shule na kamati za ujenzi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu, ikiwemo ununuzi wa milango na samani imara ili majengo yadumu kwa muda mrefu. 

Aidha Daktari Mganga, amewaagiza walimu kuongeza bidii katika ufundishaji wanafunzi ili kuinua ufaulu, sambamba na utunzaji bora wa mazingira ya shule. Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula bora chenye lishe ili kuboresha afya na uwezo wa kujifunza.

Kwa niaba ya wananchi na uongozi wa shule, Mkuu wa Shule ya Msingi Ushora Utemini, Mwalimu Julius K. Massawa, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa huruma na uwekezaji mkubwa aliofanya katika sekta ya elimu unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia wilayani humo.




 


IDADI YA WAKALIMANI LUGHA YA ALAMA KUONGEZWA,VIZIWI KUPATA STAHIKI ZAO

 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Daktari Fatuma Mganga ameagiza kuongezwa kwa idadi ya Wataalam wa lugha ya alama(Wakalimani) katika maeneo mbalimbali ya Umma ya kutolea huduma za kijamii ili kutengeneza mazingira rafiki kwa viziwi wanaposhiriki katika mikutano,vikao ili kuwawezesha kupata huduma zilizo bora sambamba na kushiriki katika kutoa maamuzi yanayaowagusa wanajamii kwa ujumla.

Hayo yamezungumzwa leo Septemba 24,2025 katika eneo la Chuo cha VETA Mkoani Singida katika Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi duniani iliyowakutanisha Viziwi kutoka mikoa yote Tanzania,wakalimani sambamba na Maafisa Elimu maalum chini ya Kaulimbiu isemayo

"Bila lugha ya alama hakuna haki za binadamu"

Daktari Mganga ametoa Agizo kwa kila halmashauri kuhakikisha kuna mtaalam wa lugha ya alama,kadhalika katika mahospitali , katika mikusanyiko mikubwa ikiwemo masokoni na mikutanoni ili kusaidia kutoa huduma inapohitajika sambamba na wao kutoa maoni ya yabayowagusa.

"Viziwi wanahitaji elimu na huuma nyingine za kijamii,hivyo ni sahihi kanzidata kufanyika vizuri ili kufahamu idadi yao vema ili kuwarahisishia kupata huduma muhimu wananchi wanazitakiwa kuzipata ikiwemo huduma za elimu kwa wote watoto na watu wazima kupitia elimu ya watu wazima,kadhalika huduma za kifedha katika benki,mikopo mbalimbali"

Kadhalika amewaagiza Maafisa ustawi wa jamii Nendeni mkahakikishe mnapata idadi kamili ya Viziwi ili kupata takwimu sahihi,lengo kuu ni kuhakikisha wote wanapata elimu kwani ndiyo msingi wa kila jambo na baadae kujiunga na elimu za Vyuo na Sekondari kadhalika kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowawezesha kujitegemea.

Aidha, ameagiza Bodi husika kuhakikisha viziwi wanapewa elimu ya uchumi na uwezeshaji ili kuweza kujikwamua kiuchumi kadhalika na kuandaa ripoti ya namna gani mmeweza kutoa matokeo chanya katika kusimamia viziwi kupata masilahi yao ikiwemo kufanya ujasiriamali na kunufaika na mikopo mbalimbali inayotolewa na Halmashauri na Wizara ambayo ni ya makundi maalum.

Sambamba amewaasa Wakalimani kuwa na maadili ya kutunza siri za viziwi kwa kuwadhalilisha kwa kutoa siri zao za ndani kwa watu wasiohusika hali inayowafanya wajisikie vibaya kwa kuona wamedhalilishwa utu wao kutokaana na madhaifu yao.

Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Daktari Samia Suluhu Hassan inawatambua na kuwajali kwa kuwapa kipaumbele viziwi kwa kuanzisha vituo mbalimbali vya kuwahudumia ikiwemo Vituo 176 nchi nzima,Vifaa vya kujifunzia kadhalika imeweka mikakati madhubuti ya kushughulikia changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi), ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa elimu jumuishi na huduma za afya rafiki kwa viziwi.

Kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Wizara ya Elimu, serikali imeongeza ajira kwa wakalimani wa lugha ya alama, kuwezesha upatikanaji wa vifaa saidizi kama vile vifaa vya usikivu na kuboresha miundombinu ya shule ili iwe rafiki kwa wanafunzi viziwi. 

Aidha, serikali imeendelea kushirikiana na mashirika ya kiraia katika kutoa elimu ya lugha ya alama kwa watumishi wa umma ili kuongeza ushirikishwaji wa viziwi katika huduma za kijamii na shughuli za kitaifa. Mikakati hii inaendana na dhamira ya serikali ya kuhakikisha usawa, ujumuishaji na ustawi wa makundi maalum katika maendeleo ya taifa.

Amehitimisha kwa kuwataka wote kutumia haki yao kikatiba ifikapo Oktoba 29,2025 kuhakikisha wanakwenda katika vituo vya kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi wa ngazi za Udiwani,Wabunge na Rais kwa ajili ya kupata viongozi bora watakaoleta maendeleo na kutetea haki za wananchi na wenye mahitaji maalum kwa ujumla hivyo wasijione wanyonge na dhaifu kwani haki ya kupiga kura ni ya kila mmoja.


Tuesday, September 23, 2025

MRADI WA MABWAWA YA KUTIBU MAJITAKA KUKAMILIKA OKTOBA,WANANCHI KUNUFAIKA.

 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, leo amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ndani ya Manispaa ya Singida, ambapo alipata fursa ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Mabwawa ya Kutibu Majitaka unaotekelezwa katika eneo la Manga, Kata ya Mtipa.


Katika ziara hiyo, Dkt. Mganga sambamba na timu ya ufuatiliaji ya Mkoa walisomewa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa na wa kimkakati, ambao unalenga kuboresha huduma za usafi wa mazingira na afya ya umma kwa wakazi zaidi ya laki moja wa Manispaa ya Singida.

Mradi huo unatekelezwa na Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Singida (SUWASA), na unahusisha ujenzi wa mabwawa matano ya kutibu majitaka kwa teknolojia ya kisasa (anaerobic, facultative & wetlands), pamoja na maabara ya kupima ubora wa majitaka yaliyotibiwa, gari la kubeba majitaka, barabara na uzio wa kuzunguka eneo la mradi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi kufikia Septemba 2025, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 71, huku mabwawa yote matano yakiwa tayari yamekamilika. Shughuli zinazoendelea ni pamoja na ulazaji wa mabomba ya kuunganisha mabwawa, ukamilishaji wa jengo la maabara, jengo la mlinzi na usimikaji wa nguzo za fensi.

Mradi ulianza kutekelezwa rasmi tarehe 16 Mei 2023, na unatarajiwa kukamilika tarehe 27 Oktoba 2025, kwa kipindi cha miezi 29 na siku 11.

Katika taarifa hiyo, ilielezwa kuwa zaidi ya wananchi 112,934 watanufaika moja kwa moja na mradi huo kwa kupata huduma bora za usafi wa mazingira. Aidha, mradi huo unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kuenea kwa magonjwa ya tumbo na kuhara yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira kutokana na utiririshaji wa majitaka usio rasmi.

Majitaka yaliyotibiwa yatatumika kwenye kilimo cha mboga mboga na matunda, hivyo kuongeza kipato kwa wananchi wa maeneo ya jirani. Vilevile, mradi unazalisha mbolea bora ya muda mrefu ambayo itapatikana kutoka kwenye mabwawa hayo, na inakadiriwa kudumu shambani kwa hadi miaka mitatu.

Zaidi ya hayo, eneo la mradi lina ukubwa wa meta za mraba 211,005, ambalo litahifadhiwa na kuendelezwa kwa upandaji miti na uboreshaji wa uoto wa asili, hatua itakayochangia kuimarisha hali ya hewa ya eneo hilo.

Dkt. Fatuma Mganga amepongeza hatua kubwa ya utekelezaji iliyofikiwa na kueleza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kufuatilia kwa karibu miradi yote ya maendeleo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.